Cheka anatarajia kusoma masomo ya Kiingereza na Biashara.
Dar es Salaam. Leo bingwa wa dunia wa WBF, Francis
‘SMG’ Cheka ataandika historia mpya ya maisha yake kwa kuanza rasmi
masomo yake ya awali ya sekondari katika shule ya St Joseph mjini
Morogoro.
Cheka anayepigania uzani wa super middle (kg 76) alifikia uamuzi wa
kurudi shule baada ya kupewa ufadhili na Shule ya Sekondali ya St
Joseph.
“Sijui masomo yatakuwaje, lakini vyovyote itakavyokuwa nitapambana
nayo kwani uamuzi wa kurudi shule umetoka moyoni hivyo sitateteleka,
lakini kabla ya kwenda shule nitaanza mazoezi kwanza,” alisema Cheka
katika mahojiano na Mwananchi.
Cheka baba wa watoto wawili, Boniface na Historia anadai alikuwa na
ndoto za kujiendeleza kielimu tangu zamani japo alishindwa kutokana na
majukumu ya kifamilia.
“Naenda kusoma kweli, sitafanya mzaha hata kidogo kwenye masomo
yangu, pia sitaacha kufanya mazoezi kwani Desemba natakiwa kutetea taji
langu la dunia,” alisema bondia huyo asiyekamatika hapa nchini kwenye
ngumi za kulipwa.
Cheka alihitimu elimu yake ya msingi miaka kadhaa iliyopita Shule
ya Msingi Kinondoni B, Dar es Salaam ambapo kwa mujibu wa bondia huyo
hakubahatika kuendelea kutokana na matatizo ya kifamilia na kujikita
kwenye ngumi za ridhaa wakati huo kabla ya mwaka 2000 kujiunga rasmi
kwenye ngumi za kulipwa.
Tangu wakati huo amefanikiwa kutwaa ubingwa wa taifa, mataji ya
Afrika ya UBO, IBO, IBF, WBC na WBO kabla ya mwishoni mwa Agosti mwaka
huu kutwaa ubingwa wa dunia wa WBF baada ya kumpiga Phil Williams wa
Marekani kwa pointi, Dar es Salaam.

No comments:
Post a Comment