

MASHITAKA
11 dhidi ya aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, yamebainisha kuwa kosa kubwa la
kiongozi huyo kijana, ni nia yake ya kutaka kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa
Taifa, Freeman Mbowe.
Chanzo chetu cha habari kilichoona
mashitaka hayo kabla ya kutumwa kwa washitakiwa, kimebainisha kuwa makosa saba
kati ya makosa 11, yanahusu kugombea uenyekiti Taifa, au kumkashifu Mwenyekiti
wa Taifa.
“Ukiona hayo mashitaka yenyewe ndugu
yangu, yanajirudia rudia na kuzunguka katika kosa moja la nia ya kuwania nafasi
ya Mwenyekiti wa Taifa… angalia kosa la kwanza,
kosa la tatu, tano, sita nane na tisa, ni kama vile kuwania uenyekiti ndio kosa kubwa.
“Hata hivyo kwa jinsi mgawanyiko
ulivyo ndani ya chama sasa, nakuhakikishia hawa jamaa (Zitto, Dk Kitila Mkumbo
na Samson Mwigamba), watarudishwa katika nyadhifa zao na hakuna
atakayeadhibiwa,” alisema mtoa taarifa wetu.
Alinukuu kauli ya Mjumbe wa Kamati Kuu
ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu
aliyehoji kama makosa wanayotuhumiwa akina Zitto ni makubwa kiasi cha kuyeyusha
mema aliyoyafanya katika chama. “Si umesikia akina Baregu wakizungumza? Kwa
mashitaka yale nakuhakikishia kitakachofanyika ni kufunika kombe mwanaharamu
apite,” alisema mtoa habari wetu.
Kosa
la kwanza kwa
Zitto, Dk Mkumbo na Mwigamba, wanadaiwa kuvunja Kanuni ya Chama
inayokataza kukashifu chama, kiongozi au mwanachama yeyote. Katika maelezo ya
kosa hilo, akina Zitto wanadaiwa kumkashifu Mwenyekiti wa Taifa, Mbowe, Katibu
Mkuu, Dk Willibrod Slaa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema.
Moja ya madai katika mashitaka hayo,
ni kilichoandikwa katika Mkakati wa Mabadiliko 2013, kuwa Mbowe amekuwa
akinunua vifaa vyote vya chama nje ya nchi kwa bei anayoijua mwenyewe na ambayo
haihojiwi popote. Wanadaiwa pia wamemkashifu Dk Slaa kwa kudai ni mdhaifu kwa
kumruhusu Mbowe kuingilia shughuli za kiutendaji.
Zitto na wenzake wanadaiwa
katika kosa la pili, kutokuwa
wawazi na wa kweli wakati wote na kushirikiana na vikundi vya majungu na
udanganyifu kinyume na Kanuni za Uendeshaji kipengele cha 10.1 (VIII.
Katika
kosa la tatu, wanadaiwa
kutoa tuhuma juu ya viongozi wenzao bila kupitia vikao halali na utaratibu wa
ngazi zilizowekwa, kinyume na kanuni ya 10.1 (X).
Katika
kosa la nne, akina
Zitto wanadaiwa kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini au
ukanda ambavyo vina makusudi ya kubaguana ndani ya chama, miongoni mwa jamii,
kisiasa au kijamii. Katika kosa hilo wanadaiwa kwenda kinyume na kipengele cha
10.1 (IV), cha Kanuni za Uendeshaji wa Chama.
Akina Zitto katika kosa la tano, wanadaiwa
kujihusisha na vitendo vya kuchonganisha na kuzua migogoro kwa viongozi wa
chama au wanachama, kinyume na kifungu cha 10.1 (IX), cha Kanuni za Uendeshaji
wa Chama.
Katika kosa la sita ambalo mtoa habari wetu alisema ndio kubwa, Zitto
na wenzake wanadaiwa kutekeleza mpango wa kusudio la kugombea uenyekiti wa
Chama Taifa, bila kutangaza kusudio la kutangaza nafasi hiyo.
Hatua hiyo inadaiwa kuwa ni kinyume na
kifungu 2.C cha Muongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi ya Uongozi wa Chama, Mabaraza na Serikali wa
2012.
Zitto na wenzake katika kosa la saba, wanadaiwa
kutengeneza mitandao ya kuwania uongozi ndani ya chama kwa nia ya
kujihakikishia ushindi kinyume na kanuni ya 2 (D), ya Muongozo wa Kuwania
Uongozi.
Katika kosa la nane, Zitto na wenzake wanadaiwa kuwachafua viongozi
na wanachama wengine wenye kusudio/nia ya kutaka kugombea nafasi ya uenyekiti
kinyume na kifungu 2 (E) cha Muongozo wa Kuwania Uongozi.
Katika kosa hilo, kumewekwa maelezo ya
ziada kuwa kosa hilo linaunganishwa na kosa la kwanza ambalo washitakiwa
wanadiwa kuwakashifu Mbowe, Dk Slaa na Lema.
Kosa
la tisa, akina
Zitto wanadaiwa kujihusisha na upinzani dhidi ya chama na makundi ya majungu ya
kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa uchaguzi wa chama, kinyume na
kifungu cha 10.3 (IV), cha Kanuni za Uendeshaji.
Kosa
la kumi linamhusu
Zitto peke yake, ambapo anaidaiwa kukashifu chama na kiongozi wa chama nje ya
Bunge kinyume na kifungu 2 C (B), kikisomwa pamoja na kifungu 3 B cha Kanuni za
Mwenendo wa Maadili ya Wabunge.
Katika hilo Zitto kwa kushirikiana na
baadhi ya viongozi wa chama yaani Dk Mkumbo na Mwigamba na mtu mwingine ambaye
hajajulikana, wanadaiwa kusambaza waraka uitwao Mkakati wa Mabadiliko 2013.
Mkakati huo, unadaiwa kukashifu chama
na/ au viongozi wake wakuu kama ilivyoelezwa katika kosa la kwanza, tatu, nne
na nane.
Mwisho katika kosa la 11, Zitto na wenzake
wanadaiwa kuchochea mgawanyiko ndani ya chama kinyume na kanuni ya 3 F ya
Kanuni za Mwenendo wa Maadili ya Bunge.
No comments:
Post a Comment