UKIFIKA katika
mtaa anaoishi mwanamuziki Diamond maeneo ya Sinza Mori jijini Dar es Salaam
utaanza kuhisi kuwa kuna staa anayeishi maeneo hayo, macho ya wengi huanza
kumtazama mtu anayeelekea katika geti la nyumba anayoishi msanii huyo. (HM)
Muda wote
geti hilo limefungwa. Ili uweze kuingia ndani itakulazimu ubonyeze kengele
itakayoashiria kuwa kuna mgeni nje anahitaji kuingia ndani. Hata hivyo hauwezi
kupenya kirahisi ndani hadi uulizwe shida yako na kama hauna miadi na mtu
yeyote anayeishi ndani ya nyumba hiyo haitakuwa rahisi kuingia.
na kushuhudia ukimya wa hali ya juu ilhali kuna watu
ndani. Baada ya kufunguliwa geti tuliingia ndani na kupokewa na Diamond
aliyekuwa ameketi katika sebule iliyonakshiwa na mapambo makini ukutani huku
ikiwa na samani chache lakini za gharama kubwa.
Tulitumia saa mbili mfululizo katika mahojiano na Diamond
ambaye alifunguka kwa kila swali aliloulizwa na kujibu kwa ufasaha na ufafanuzi
mpana.
Mwanaspoti: Utendaji
kazi wako ukoje katika muziki?
Diamond: Nina mipango makini katika kazi
zangu. Mambo yote lazima yapitie kwa meneja wangu ndipo yanifikie mimi, mara
nyingi mtu hawezi kuzungumza na mimi moja kwa moja lazima apite huko na hiyo
ndiyo staili ya Diamond. Nimejipanga kuhakikisha nafanya kazi gani, kwa wakati gani
na sikurupuki tu, japo katika utengenezaji wa nyimbo zangu naweza nikapata wazo
basi hapo hapo nikatengeneza mistari.
Mwanaspoti: Utendaji kazi wako ukoje kuanzia
asubuhi hadi jioni?
Diamond: Saa tano asubuhi, nikishaamka
kitu cha kwanza ni kwenda 'gym', mara nyingi ni hapa nyumbani kama unavyoona
hapo nje kuna sehemu ya mazoezi na sehemu
nyingine
zilizopo ndani, mara nyingi hutumia muda wa saa moja. Ifikapo saa sita na nusu
huwa naanza kufanya kazi zangu lakini itategemea na ratiba zangu za siku ambazo
ndio mwongozo wangu wa kuimaliza siku. Baada ya hapo napumzika kwa muda fulani
na baadaye jioni huendelea na kazi na mara nyingi kazi zangu huwa nazimaliza
usiku wa manane.
Mwanaspoti: Unalala
saa ngapi? Na unalala kwa muda gani?
Diamond: Muda
wangu wa kulala mara nyingi ni saa kumi na moja alfajiri na kama sikuwa na kazi
nyingi studio basi nitalala saa nane usiku. Muda wangu wa kulala ni saa sita
mpaka nane kwa siku. Ila hata kama nikilala mapema kuamka ni saa tano asubuhi
ila itategemea na nini ninakifanya siku inayofuata na kama nina kazi maalumu na
ya mapema itanilazimu niamke mapema ili kuzikamilisha.
Mwanaspoti: Shughuli
gani zinazokuchelewesha mara kwa mara kulala?
Diamond: Ni kurekodi na wakati mwingine
shoo. Kwa wiki ninafanya shoo nyingi, kama ni tatu basi siku zote tatu nitalala
alfajiri. Siku nyingine zinazosalia ninalala usiku wa manane kwa kuwa huwa
nakuwa studio na sehemu nyingine ambazo hunilazimu kufanya kazi kwa kipindi
kirefu usiku.
Mwanaspoti: Kati ya usiku na mchana ni muda
upi unaopenda kurekodi?
Diamond: Kazi zangu narekodi usiku na
ndiyo muda ninaopendelea zaidi. Mara nyingi napenda kurekodi saa 7 usiku ili
niwe na muda na saa nyingine ni kuepuka lawama kurekodi mchana, kwasababu
vijana wengi chipukizi wataona napendelewa. Unajua ninapoingia studio napenda
kufanya kazi kwa muda mrefu, hata hivyo iliyo bora sifanyi bora liende na
siwezi kufanya kazi na prodyuza anayenipeleka tu, ni lazima na mimi nipime kama
kazi niliyoifanya inakwenda vile ninavyotaka au kama yeye anavyotaka ilimradi
tufanye kazi nzuri na iliyo bora.
Mwanaspoti: Unatumia muda gani kurekodi
singo moja na kwa upande wa video ni siku ngapi?
Diamond: Inategemea, inaweza kuwa siku
mbili au miezi sita lakini nyimbo nyingi zinatumia muda mwingi kwasababu wakati
mwingine naanza halafu napata shoo hivyo inanibidi nipange muda mwingine wa
kurekodi. Kuna nyimbo zangu ambazo nilizifanya kwa muda mrefu sana hizo huwa
sizisahau ikiwemo Ukimwona, Mbagala, Nataka Kulewa na nyinginezo. Nakumbuka
katika kazi nilizofanya kwa muda mfupi ni My Number One nilioufanya kwa
prodyuza Sheddy Clever kwa kipindi kifupi sana pamoja na Mapenzi Basi sambamba
na Binadamu hizi ni baadhi ya kazi ambazo hazikunipasua sana kichwa
kuzikamilisha.
Mwanaspoti: Una
prodyuza wako maalumu au studio yako mwenyewe?
Diamond: Sina prodyuza maalumu kila kazi
nitakayotaka kuifanya ninatafuta prodyuza yule ninayemtaka hata kama sijawahi
kufanya naye kazi. Ninafanya hivi nikiwa na malengo maalumu kwa kujiweka vizuri
mimi kama msanii na hata kuwapa nafasi maprodyuza mbalimbali kutia mkono kwenye
kazi ya mikono yangu. Ninaogopa kuwa na prodyuza maalumu kwa kuwa najua
atanisumbua ikiwa atajua kwamba namtegemea yeye pekee katika kazi zangu. Studio
sina kwa sasa ila nina mikakati ya kuwa na studio kwani nimeshanunua baadhi ya
vifaa.
Mwanaspoti: Unadhani ndiyo sababu
iliyokufanya ukagombana na Bob Junior au Manecky?
Diamond: Hapana haya mambo yalishapita
lakini nilijifunza mengi ndiyo maana niliamua kuja na staili hii. Naogopa
kubaki kuwa msanii ninayetegemea prodyuza fulani, bila yeye siwezi kufanya muziki,
lakini mimi ni Diamond ninaweza kufanya muziki na prodyuza yeyote naye
akaonyesha ufundi wake kupitia kazi yangu.
Mwanaspoti: Shoo gani kubwa kuliko zote
uliyowahi kufanya ambayo haijawahi kujirudia?
Diamond: Diamond Forever. Hii ilikuwa
kubwa sana ambayo sitakaa nikaisahau, ilihudhuriwa na watu wakubwa na maarufu
hapa nchini hata hivyo ilikuwa ya kipekee ambayo haijafanana na yoyote ile. Ya
pili ni ile ya Dar Live ambayo nilifanya baada ya kushuka katika helikopta ile
pia ilikuwa kubwa. Lakini kwa nje ya nchi ni Mombasa na Comoro huko nilifanya
shoo kubwa sana ambazo siwezi kuzisahau.
Mwanaspoti: Ni shoo ipi iliyowahi
kukuingizia pesa kubwa kuliko zote?
Diamond: Shoo ile ya Mlimani City ya
Diamond Forever, ile iliniingizia pesa kubwa sana na tangu pale ndipo
nilipoanza kufurahia matunda ya kazi yangu. Nilifanya shoo pia Burundi, Mombasa
na Congo shoo hizi ziliniingizia kiasi kikubwa sana cha pesa siwezi kutaja ni
shilingi ngapi lakini ni pesa nyingi ambazo sitakaa nizisahau.
Mwanaspoti: Shoo ipi ilikuwa ya bei chee
ambayo huwezi kuisahau
Diamond: Kwa kweli siwezi kusahau
nilipofanya shoo yangu ya kwanza kubwa mwaka 2009 kwenye Fiesta iliyofanyika
Dar es Salaam, ilikuwa ndiyo shoo yangu ya kwanza na kubwa wakati huo nilikuwa
natamba na wimbo Kamwambie, ilinichukua muda mrefu sana kujiandaa mimi pamoja
na madansa wangu wanne tulilipwa Sh 50,000 lakini sikukata tamaa kwani ilikuwa
ndiyo mwanzo wangu wa kujuana na watu wengi na wadau wakubwa wa muziki hapa
nchini ambao nilikutana nao kwenye ile shoo.
Mwanaspoti: Kwa hivi sasa ni shoo gani
ambayo unaweza kusema kwamba utafanya kwa bei ya chini na ni shilingi ngapi?
Diamond: Shoo ninayoweza kufanya kwa bei
ya chini kabisa ni Sh 10 milioni za Kitanzania na hii labda nione anayeniomba
nifanye shoo hiyo hayuko vizuri na pengine ni rafiki yangu na hawezi
kuninyonya, si hivyo tu itategemea pia ni kampuni gani na ni watu wa aina gani
ambao watanitaka nifanye nao kazi.
Mwanaspoti: Kwa kawaida Diamond ni msanii wa
gharama gani kwa shoo moja ndani na nje ya nchi?
Diamond: Kwa kawaida shoo moja ninafanya
kuanzia Sh15 milioni mpaka Sh20 milioni kulingana na muda nitakaofanya shoo.
Pia zile za nje ninafanya kwa gharama ya Dola 20,000 mpaka 30,000 yaani ni Sh32
milioni mpaka 48 milioni hivi kwa fedha za Tanzania na nikiwa huko nahakikisha
ninafanya kazi vile inavyotakiwa. Lakini hali ni tofauti inavyokuja shoo ile ya
uwanjani yaani hapa nazungumzia shoo kubwa zinazofanyika nje ya ukumbi, hizi
natoza Dola 20,000 ambayo ni sawa na Sh32 milioni 32 kwa fedha ya Kitanzania.
Mwanaspoti: Kuhusu madansa wako
unawachukuliaje?
Diamond: Ni kama kaka zangu na
ninawapenda sana kwani tumetoka nao mbali na wanajua kuwa tunafanya kazi pamoja
kutengeneza maisha hivyo ni kama ndugu zangu na tunasaidiana kwenye kila jambo
ukizingatia kuwa kile tunachokipata tunagawana. Kwa kweli najitahidi sana
kuwaambia hasa kuhusiana na masuala ya kimaisha, nahusika katika maisha yao ya
kila siku na nijuavyo mimi nikikosea tu mmoja akapotea kundi langu litakuwa
limeharibikiwa maana kila mtu namtegemea kwa upande wake. Kwa sasa wamejenga
nyumba zao na wanaendelea vizuri kimaisha hilo ndilo sharti langu lazima
wafanye mambo ya maendeleo kwa kile tunachokipata.
Mwanaspoti: Umesafiri nao nchi ngapi, na
kwanini unapenda kuambatana nao?
Diamond: Nimesafiri nao sehemu mbalimbali
kama Burundi, Comorro na sehemu nyinginezo ambako nimekwenda kufanya shoo, sina
tabia ya kusafiri peke yangu hata nikienda Ulaya na hata Marekani lazima niwe
nao. Ninapenda kuwa nao kwani ni sehemu ya muziki wangu na imefika wakati
nimekuwa nataka mapromota kuhakikisha wanatulipia mimi na madansa wangu kwa
ajili ya shoo hasa tutakapojua kuwa shoo fulani itaingiza watu wengi au
udhamini mkubwa.
Mwanaspoti: Kuna
safari ambayo umewahi kusafiri peke yako?
Diamond: Ziko nyingi, nilienda mwenyewe
kutokana na ukubwa wa shoo, lakini ni miaka kadhaa nyuma, baadaye nilijiwekea
mikakati kwamba siwezi kusafiri mwenyewe wakati shoo nahitaji kufanya na
madansa wangu, awali mapromota walikuwa wagumu kunielewa na wapo waliokataa.
Niliachana nao na kuwataka wakishajipanga na kuhakikisha kwamba wanaweza
kunichukua mimi na madansa wangu watafanya hivyo.
Mwanaspoti: Umewahi kuwatema madansa?
Diamond: Sijawahi kubadilisha madansa kwa
sababu wanajua kazi yao. Ingawa nilikuwa na madansa sita nilipokuwa naanza
muziki lakini niliachana na wawili kutokana na utendaji wao wa kazi. Wawili
hawa hawakuwa wabunifu kila siku walikuwa na staili ileile, niliamua kuchagua
vichwa ambavyo vikikaa na mimi mwishowe tunatoka na kitu makini na chenye
kueleweka. Kulikuwa na tatizo pia la kukosea stepu wakati wa shoo hili lilikuwa
likinishushia sana hadhi yangu jukwaani, hapo ndipo nilipoamua kuwaondoa.
Mwanaspoti: Kwa upande wa malipo
unawalipaje?
Diamond: Ninawalipa vizuri lakini siwezi
kutaja kiwango ila ingekuwa kwangu ningetaja, hiyo ni haki yao wao wenyewe
kutamka ila mimi siwezi kutaja. Malipo ninayowalipa yapo machoni mwa watu
wanaowazunguka, dansa kujenga nyumba kumiliki baadhi ya biashara si jambo dogo,
hivyo ninawalipa vizuri. Na hata gharama za kusafiri ndani na nje ya nchi vyote
ni juu yangu, malipo tunayoyapata tunagawana.
Mwanaspoti: Unakumbana
na changamoto zipi katika kazi yako?
Diamond: Nakumbana na mengi, kwanza
unapokuwa msanii unayeongoza lazima upate vikwazo vingi. Nakumbana na watu
wengi wanaonichukia na kunitusi bila sababu za msingi, hata hivyo nasingiziwa
vitu vingi ambavyo havipo nadhani hii ni changamoto iliyotokana na kufanya vizuri
katika muziki.
Wapo ambao
wanamwona Diamond anafanya vizuri kwenye muziki badala ya kukaa na kuangalia
nimepita wapi na wapi anaanza kutoa lawama kwamba ameibiwa na mengine ambayo
kimsingi hayana maana.
Mwanaspoti: Siku za hivi karibuni kuna
maprodyuza na wasanii wasiofahamika ambao walijaribu kutengeneza kazi yako ya
My Number One na kukutusi kupitia wimbo huo na wapo waliotunga mashairi mengine
yaliyozungumzia maisha yako kabla hujawa staa, ulijisikiaje? Na unachukua hatua
gani?
Diamond: Awali niliumia sana nilipoibiwa
mashairi ya wimbo wangu wa Mbagala, iliniuma sana kwa muda wa wiki nzima
uchungu nilioupata siwezi kuuelezea. Lakini baadaye nilikomaa, huwezi amini
niliposikia zile nyimbo nilicheka sana kisha nikawadharau sana watu waliofanya
hivyo maana nipo kwenye hii tasnia siwezi kuchukia watu wasiojua walitendalo
kwani na wao wapo katika kujitafutia riziki. Lakini hata hivyo sheria ya muziki
bado haijawa makini hapa nchini
nitachukua hatua gani mwisho wa siku
nitaacha kufanya mambo yangu ya msingi na kushughulikia wezi wa kazi zangu
ambao hata hivyo hawatabanwa kwa lile walilolifanya.
Mwanaspoti: Msanii yupi hapa Tanzania
anakutisha kama hayupo vipi huko nje ya nchi?
Diamond: Kwa hapa Tanzania sijaona
mwanamuziki anayenitisha, ila siwezi kujua mashabiki wao ndio majaji, nafikiri
kila mtu anaweza kuwa na mtazamo wake. Kati ya wanamuziki ninaowahusudu mimi
kwa nje ya nchi hasa Afrika ni P Square pekee, hawa wapo katika nafasi kubwa
sana kwenye ubongo wangu na nafikiria ni lini ninaweza kuwafikia, hiyo ndiyo
ndoto yangu daima.
Mwanaspoti: Unapokuwa juu ya jukwaa
unakumbana na vishawishi vipi ukiwa kama msanii mkubwa?
Diamond: Ninapata vishawishi vingi sana
ninapokuwa jukwaani. Kwa kweli ninashawishiwa na wakinadada, mfano kuna
mwanamke mmoja ambaye alikuwa mmoja wa mapromota wa shoo nchini Uingereza
alitaka kunibusu mdomoni kwa lazima, kitendo kile kilinifedhehesha sana na nilishindwa
nifanyeje kwani nipo ugenini na jukwaani ilikuwa ngumu sana kwangu. Wakati
mwingine wanawake wanapanda jukwaani ili wacheze na wewe mwisho wa siku
wanaingiza mikono kwenye suruali yaani sipendezwi kabisa na michezo ya namna
hii.
Mwanaspoti: Umewahi kuibiwa ukiwa
jukwaani?
Diamond: Nimeshaibiwa sana hasa katika
hizi shoo ndogo ndogo mara nyingi watu wanapanda jukwaani na kuondoka na kitu
chako. Nakumbuka nimeshawahi kuibiwa saa, pete ya dhahabu na kuna mmoja alitoa
kali ya mwaka yaani yeye alinivua nguo kwa lazima.
Mwanaspoti: Inakuwaje nje ya
muziki, unakumbana na changamoto zipi?
Diamond: Kitu ambacho ni changamoto kubwa sana kwangu ni
simu yangu ya mkononi. Kila baada ya miezi sita au mitatu nalazimika kubadili
namba yangu ya simu, nasumbuliwa sana na watu ambao hata hivyo hawana la msingi
la kuniambia. Ni kweli kwamba mawasiliano ni kitu cha msingi na
ninawapenda
mashabiki wangu lakini namba yangu inasambaa kwa kasi ya ajabu kiasi kwamba
nashindwa kupokea simu za maana kwa kudhani kwamba na hao nao ni wasumbufu.
Mwanaspoti: Ina maana milio yote ya simu
hapo ni watu wanakupigia?
Diamond: Yap, unavyoona inalia kila
dakika watu wanapiga hapa. Muda mwingi hii simu ninaweka 'silent' yaani haitoi
mlio wowote kwani inaita kila dakika.
Mwanaspoti: Tuzungumzie uhusiano wako. Mpenzi
wako wa kwanza unamkumbuka? na je uliwahi kumpa shilingi ngapi?
Diamond: Mpenzi wangu wa kwanza kabisa
enzi hizo ninajifunza mambo haya sikumbuki vyema jina ila alikuwa anaishi
Tandale na mimi pia nilikuwa naishi huko na mama yangu. Sikumbuki kama nimewahi
kumhonga maana enzi hizo mimi nilikuwa napewa tu na mama yangu pesa, sikuwa na
hela yoyote ya kumpa na ilikuwa ni kwa kipindi kifupi kama miezi minne hivi,
hata hivyo tulikuwa tunaibana tu kwa siri nilikuwa mdogo.
Mwanaspoti: Kwanini mliachana?
Diamond: Kwanza nilikuwa sijajua mapenzi
ni nini. Hata hivyo haikuwa rasmi na wala nilikuwa sijawa na akili ya kupenda
sana na nilikuwa na fikra kwamba ni mchezo tu hivyo tuliachana mapema kwani
hata yeye akili yake ilikuwa haijakomaa.
Mwanaspoti: Mpenzi wako uliyekuwa naye kabla
ya kuwa staa nasikia uliachana naye baada ya kutoka kimuziki kwa nini?
Diamond: Nilimpenda sana lakini aliniacha
kabla ya kutoka. Mpenzi wangu wa kwanza alikuwa anaitwa Sarah Sadick, sijawahi
kumuhonga na ndiye mwanamke niliyewahi kumpenda sana. Wakati huo Naseeb Abdul
kabla sijawa Diamond nilikuwa nahaha kuhangaika ni vipi nitatoka kimuziki.
Msichana huyu ndiye aliyenipa hasira za kufanya muziki kwa bidii zote baada ya
kunitema na kuanza kuhangaika na wengine na aliniita majina mengi yasiyo
mazuri, kisa sina fedha. Si kwamba nilimuacha bali yeye ndiye aliyeniacha kama
zali baada ya wiki kadhaa nikatoka na wimbo Kamwambie, taratibu nikaanza kuwa
staa naye akaanza kurudi ila nilishamuondoa moyoni mwangu.
Mwanaspoti: Kwa nini mliachana? Unadhani
hakukufaa tena kwa kuwa ulishakuwa staa?
Diamond: Alinisumbua sana kutokana na
ugumu wa maisha niliokua nao kwa kipindi cha nyuma hadi kufikia 2009.
Nilimpenda sana huwezi amini nilikuwa silali usingizi kwa ajili yake. Nahisi ilitokana
na mimi kukosa kazi ndiyo maana ilifikia hatua alinipotezea. Lakini baada ya
kupata na kujulikana alinifuata lakini sikutaka tena hata baada ya kuniomba
msamaha.
Mwanaspoti: Umewahi kuwa na
wanawake wangapi tangu uwe staa?
Diamond: Sikumbuki kwa kweli wapo wengi
mno, si unajua tena wapo walionitaka na kunilazimisha nifanye hivyo, lakini
idadi kamili siwezi kukumbuka na kila siku nasumbuliwa na hawa wanawake.
Mwanaspoti: Ni wapenzi wangapi
ambao umekuwa nao kipindi kirefu na kuwapenda kama wapenzi wako?
Diamond: Nimewahi kuwa na wapenzi
wanne katika kipindi chote cha ustaa wangu na sikupenda kubadili ovyo ila wengi
wao hawakuweza kutimiza haja ya moyo wangu.
Mwanaspoti: Unaweza kuwataja majina?
Diamond: Ndiyo ila wawili
wanafahamika zaidi. Wa kwanza kabisa alikuwa anaitwa Sarah na wa pili alikuwa
anaitwa Hawa yule msichana niliyeimba naye katika wimbo 'Nitarejea', huyu
alizidiwa ujanja na Wema Sepetu ambaye naye alikuja kuondoka kwangu na baadaye
nikawa na Penieli Mungilwa.
Mwanaspoti: Mwanamke yupi unahisi
ulimpenda kuliko wote?
Diamond: Mwanamke wangu wa kwanza Sarah
Sadick huyu aliniingia sana moyoni sijajua ni kwanini. Lakini nahisi huenda kwa
kuwa awali alinipenda kweli kwa kuwa wakati huo sikuwa na kitu. Hata hivyo
nahisi ilitokana na mimi kutokuwa bize na wakati huo sikufikiria lolote zaidi
ya yeye ilitokana na kutokuwa na kazi ya kufanya. Siku hizi sina mapenzi ya
kivilee, nawaza zaidi pesa na ninaihangaikia na zaidi ni muziki wangu, hili
ndilo la kwanza kabisa linalonifanya niwe bize mapenzi baadaye.
Mwanaspoti: Umeshawahi kutongozwa
na wanawake?
Diamond: Ndiyo, wengi sana tena kuna
mmoja kati ya wanawake niliowahi kuwa nao alinitongoza yeye mwenyewe ndipo
nikawa naye na nilikaa naye katika uhusiano kwa kipindi kirefu tu. Wanaweza
kumfikiria mwanamke fulani lakini huwezi amini ukweli ninao mimi mwenyewe na
katu hawawezi hata kumhisi. Ninatongozwa sana kwenye mitandao ya kijamii,
facebook, whatsapp, Instagram na kwingineko na wapo wasichana ambao wanatafuta
namba zangu za simu na kuanza kunisumbua.
Mwanaspoti: Unapata usumbufu
wowote toka kwa wanawake?
Diamond: Ndiyo, wengi sana tena kuna
mmoja kati ya wanawake niliowahi kuwa nao alinitongoza yeye mwenyewe ndipo
nikawa naye na nilikaa naye katika uhusiano kwa kipindi kirefu tu. Wanaweza
kumfikiria mwanamke fulani lakini huwezi amini ukweli ninao mimi mwenyewe na
katu hawawezi hata kumhisi. Ninatongozwa sana kwenye mitandao ya kijamii,
facebook, whatsapp, Instagram na kwingineko na wapo wasichana ambao wanatafuta
namba zangu za simu na kuanza kunisumbua.
Mwanaspoti: Ni mwanamke wa aina gani unataka
awe mkeo?
Diamond: Kwanza ninahitaji aijue kazi yangu na ajue
kwamba mimi ni mtu maarufu hivyo akubaliane na changamoto mbalimbali
atakazokumbana nazo kwa kipindi atakachokuwa ndani ya ndoa, siyo siku mbili
anafungasha virago. Pia ajue kwamba nitamsikiliza mama yangu kwanza kabla ya
yeye hilo naliweka wazi, yeye ana nafasi yake katika maisha yangu lakini mama
yangu nimempa kipaumbele, tatu awe tayari kuishi na mama yangu. Nne awe na
akili na mwenye utambuzi na atakayeniongoza katika kazi zangu, sihitaji.
No comments:
Post a Comment