Baada ya kusema hayo,
niwashukuru sana Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Jaji Joseph Sinde Warioba kwa
hotuba zao nzuri walizozitoa mbele ya Bunge Maalum la Katiba, wakati wa
uwasilishwaji wa rasimu na uzinduzi rasmi wa chombo hicho.
Hakika, lilikuwa ni jambo la kufurahisha sana kuwaona
viongozi hao wakitoa hotuba ambazo ziliwavutia sana watu waliozisikiliza, kwani
kila mmoja alijenga hoja kwa umahiri wa hali ya juu, kiasi cha wananchi kuzidi
kuchanganyikiwa kuhusu mustakabali wa taifa letu, hasa kwa masuala nyeti kama
yale yanayohusu muungano wetu.
Kwa maoni yangu, wote wawili walikuwa na hoja kwa
wanachokiamini, kilichobaki ni kuwaachia wajumbe wa Bunge Maalum kuchuja pumba
na mchele, ili Mtanzania ale wali safi usio na chenga.
Hata hivyo, pamoja na wajumbe kuwa na jukumu hilo zito mbele
yao, bado hawa hawawezi kufanikiwa kama Mwenyekiti wao, Samuel John Sitta na
Makamu wake, Samia Suluhu Hassan hawatawaongoza kuijadili rasimu hiyo kwa
kufuata misingi ya haki, usawa na kuweka mbele masilahi ya nchi, bila kujali
itikadi zao za kisiasa.
Sitta alijijengea heshima kubwa sana wakati akiwa Spika wa
Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwani aliliendesha vizuri,
kwa haki na bila upendeleo. Aliruhusu mijadala yenye tija kwa taifa na kamwe
hakuitetea serikali bungeni, licha ya ukweli kwamba chama chake ndicho kiliunda
serikali.
Lakini napenda kumweleza mzee Sitta kuwa Bunge la Katiba ni
zaidi ya lile alilomwachia mama Anne Makinda. Hili linazungumzia uhai wa taifa
letu, siyo tu kwa sisi tulio leo, bali kwa vizazi vyetu vijavyo. Ni bunge la
kihistoria na heshima aliyoipata ya kuliongoza, ni tunu ya pekee kwake.
Ni lazima aelewe, ndani ya Bunge hilo kuna wajumbe kutoka
makundi mbalimbali, bila shaka kila moja litataka kuwasilisha na kutetea
masilahi yao binafsi, yenye kukidhi matakwa yao. Ni sawa, waache watetee
makundi yao. Sisi tunamtaka achuje, aweke mbele kwanza masilahi ya taifa, kama
alivyofanya wakati ule akiwa Spika.
Ni yeye pekee ndiye anayeweza kutuongoza kuelekea kupata
katiba tunayoitaka. Rai yangu kwake ni kumtaka kuwa makini kama wengi
wanavyomtarajia. Ninajua hata yeye ni mfuasi wa kundi mojawapo linalotaka baadhi
ya mambo yao yapitishwe. Ninaomba busara imuongoze kutambua kuwa taifa lina
maana zaidi kuliko chama chake cha siasa.
Aruhusu hoja zitawale, hata kama hazitalipendeza mojawapo ya
kundi. Asimamie kanuni vizuri na atoe nafasi hata ya wachache kusikika. Tunajua
bunge hili siyo la mwisho kuipitisha katiba mpya, kwa sababu baada ya wao
itabidi ipigiwe kura ya maoni na wananchi. Lakini endapo wao wataikosea katika
kuijadili na kuipitia, maana yake ni kwamba wananchi watapigia kura katiba
mbovu.
Ikipitishwa katiba mbovu, hii ndiyo itakayokuwa sifa ya
Samuel Sitta, kama mwenyekiti wa bunge hili. Vizazi vijavyo vitawahukumu
wajumbe wa bunge hili, hasa aliyewaongoza kupitisha kitu ambacho kitawaletea
matatizo badala ya manufaa kama tunavyotarajia.
Kwa hadhi aliyojijengea wakati ule akiwa spika, ni wazi
kwamba wananchi wana imani kubwa na utendaji wake na wengine wakaenda mbali
zaidi na kudai kuwa anafaa kuwa rais wa nchi. Hatutaki upendeleo, uoga wala
hujuma. Hatutaki mtu yeyote atoke ndani ya ukumbi huo baada ya kazi yao
kumalizika huku akijitangaza kuwa ameshinda.
Ikitokea kundi moja kujitangazia ushindi, tujue tumeshindwa
kupata katiba bora. Itapendeza siku ya mwisho, watu wote watoke
wakitabasamu kuonyesha wao kama taifa, wameibuka washindi! Lakini wakumbuke pia
kuwa wameahidi mbele ya Mungu kuwa watajadili bila upendeleo, atakaekiuka
atakuwa amemkufuru Mungu na asubiri mapigo yake.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
No comments:
Post a Comment